Nywele za binadamu kutumika kusafisha mazingira

0
260

Taasisi isiyo ya kiserikali inayofahamika kama Dung Dung imekuja na mfumo wa kusafisha mazingira kwa kutumia nywele za binadamu.

Taasisi hiyo imeanzisha mpango unaojulikana kama ‘hair recycle project’ ambapo vipande vya nywele hukusanywa kutoka kwa watengeneza nywele na kuviweka kwenye mashine ambayo huvigeuza kuwa mfano wa mkeka ambao hutumika kunyonya mafuta na hidrokaboni nyingine zinazochafua mazingira.

Mfano huo wa mkeka wa nywele huwekwa kwenye mifereji ya maji ili kunasa uchafu kwenye maji kabla ya maji hayo kufika kwenye mito, maziwa au bahari. Nywele hizo hutumika pia kukabiliana na matatizo ya uchafuzi wa mazingira uliosababishwa na mafuriko.

MATUMIZI MENGINEYO

Nywele pia zinaweza kubadilishwa kuwa mifuko ambayo ni rafiki kwa mazingira ‘bio-composite bags’ pamoja na kutumika kusafisha mafuta yaliyomwagika.

Inakadiriwa kuwa kilo moja ya nywele inaweza kunyonya lita saba hadi nane za mafuta na hidrokaboni.

Vilevile matumizi ya nywele hutegemea na urefu wake. Rasta ndefu hubadilishwa kuwa wigi, wakati nywele fupi hufanyiwa matumizi mengine kama vile matumizi ya mbolea kwa ajili ya bustani.

Huko nchini Singapore mwaka 2021 maabara katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Nanyang (NTU) kilikuza mazao mbalimbali ya mboga za majani kwa kutumia nywele zilizotupwa baada ya kuzikusanya kutoka saluni.

Hata hivyo baadhi ya kampuni zinajaribu kutumia nywele kama nyenzo ya ujenzi.