Chongolo ashauri kompyuta liwe somo la lazima VETA

0
521

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameshauri vyuo vyote vya ufundi stadi nchini vifundishe somo la kompyuta kama somo la lazima, ili kuendana na teknolojia na mahitaji ya sasa ya dunia.

Chongolo ametoa ushauri huo wilayani Ikungi mkoani Singida alipokagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi wilayani humo (Ikungi DVTC) unaotekelezwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Amesema ni vema vyuo vyote vya ufundi nchini kuona haja ya kufanya somo la kompyuta kuwa somo la lazima kwa wanafunzi wote wanaosoma katika vyuo hivyo ili wapate ujuzi wa kutumia kifaa hicho na kuendana na soko la dunia la sasa linalohitaji wanataaluma wenye ujuzi na weledi.

“Nishauri vyuo vyote vya ufundi kuona haja ya kufanya somo la kompyuta kuwa somo la lazima kwa wanafunzi wapate ujuzi waendane na mabadiliko ya dunia ya sasa,” ameshauri Chongolo

Chuo hicho cha Ikungi DVTC kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 240 wa kozi ndefu na wengine wa kozi fupi na kitakuwa na bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 144.

Gharama za utekelezaji wa mradi huo ni zaidi ya shilingi bilioni 2.3.