Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Tanzania itapata faida nyingi za kiuchumi endapo itaridhia Mkataba wa uanzishwaji wa eneo huru la Biashara la Afrika(AfCFTA).
Prof. Mkumbo ameyasema hayo akijumuisha maoni na mapendekezo ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira wakati wa semina iliyolenga kuwaelimisha wajumbe wa kamati hiyo kuhusu mkataba huo iliyofanyika Septemba 3, 2021 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Amesema Serikali imeshafanya uchambuzi wa faida na hasara za mkataba huo na kujiridhisha kuwa faida ni kubwa kuliko hasara iwapo Tanzania itaridhia kujiunga na mkataba huo.
“ Serikali imefanya tathimini na kuona kuna faida kubwa ya kiuchumi nchi ikijiunga, na kisisani nchi yetu inajulikana kuwa mstari wa mbele kwenye ukombozi hivyo hatuwezi kurudi nyuma katika ukombozi wa kiuchumi.” Alisema Prof. Mkumbo.
Akitaja faida hizo, Profesa Mkumbo amesema, kupatikana kwa masoko mapya ya mazao ya kilimo na hivyo kuchochea uzalishaji wake nchini, Kuimarika kwa mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo ambayo mengi yanahusisha wakulima wadogo kama vile alizeti, pamba, karafuu, viungo, matunda na mbogamboga kutokana na kuongezeka kwa soko la bidhaa ambazo zitazalishwa nchini na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.
Faida nyingine zilizotajwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji na ajira kwa wakulima na wadau wanahusisha katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, Upatikanaji wa bidhaa za aina mbalimbali (varieties) nchini na kupatikana kwa soko kubwa la bidhaa na huduma lenye idadi ya watu takriban bilioni 1.2 ukilinganisha na idadi ya watu takribani milioni 522 katika nchi za EAC na SADC.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mtangamano wa Biashara katika Wizara hito Ally Gugu akiwaelimisha Wajumbe hao amesema Mkataba huo unahusisha maeneo ya ushirikiano katika Itifaki ya Biashara ya Bidhaa, Huduma, Usuluhishi wa Migogoro, Uwekezaji, Haki Miliki Ubunifu, Sera za Ushindani, na Biashara Mtandao (E-Commerce).