Tani 22 za samaki zasafirishwa kwenda Ubelgiji

0
775

Wafanyakazi wa viwanja vya ndege nchini wametakiwa kubadilika kuendana na maboresho yanayofanyika katika viwanja vya ndege nchini ili kukidhi viwango vya kimataifa vya huduma za usafirishaji.

Wito huo umetolewa na mkuu wa mkoa wa Mwanza, –  John Mongela wakati akizungumza na wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa Mwanza mara baada ya kushuhudia shehena ya tani 22 za minofu ya samaki zikisafirishwa kwenda nchini Ubelgiji kupitia shirika la ndege la Rwanda.

Amesema idadi ya ndege itazidi kuongezeka nchini ili kukidhi mahitaji ya soko, hivyo ni lazima wafanyakazi wa viwanja vya ndege nao wakabadilika katika utendaji kazi.

Kwa upande wao, baadhi ya wamiliki wa viwanda vya samaki jijini Mwanza wameelezea kufurahishwa na maboresho yaliyofanyika katika uwanja wa ndege wa Mwanza na kuiomba serikali kuongeza idadi ya ndege kwa kuwa uzalishaji wa samaki unazidi kuongezeka. 

Wiki iliyopita Tanzania ilisafirisha takribani tani 20 za samaki pamoja na mabondo ya samaki kwenda katika mabara ya Ulaya na Asia kupitia shirika la ndege la Ethiopia.