SIDO yatakiwa kubuni teknolojia na mitambo rafiki

0
2132

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Nchini (SIDO) kujielekeza katika kubuni teknolojia na mitambo rafiki inayolenga kutatua changamoto za wajasiriamali kulingana na mazingira yao.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akifungua maonesho ya SIDO kitaifa yanayofanyika kwenye viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani Simiyu na kuhudhuriwa na wajasiriamali takribani mia tano.

Amesema  kuwa serikali inaendelea kuimarisha shughuli za SIDO lakini bado kuna  changamoto za wajasiriamali wadogo ambazo lazima zishughulikiwe kwa kasi kubwa ili kufungamanisha shughuli za shirika hilo na uchumi wa viwanda

Waziri Mkuu ameongeza kuwa, ili kufikia uchumi wa kati inambidi kila Mtanzania mahali alipo afanye kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu.

“Tusipoteze wakati kwa kufanya mambo yasiyo na tija, tuzingatie falsafa ya serikali ya awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu, fano kwa hapa Bariadi, tunatarajia SIDO watuletee teknolojia na mitambo inayoweza kurahisisha ukamuaji wa mafuta yanayotokana na mbegu za alizeti na pamba, kwa Dodoma teknolojia na mitambo kwa ajili ya kuchakata zabibu,”ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesisitiza kuwa ili nchi iweze kupata mafanikio, SIDO inatakiwa iwaunganishe wajasiriamali na taasisi mbalimbali za fedha ili wapate mikopo yenye masharti nafuu.

Pia, Waziri Mkuu Majaliwa amewasihi wajasiriamali wanaoshiriki maonesho hayo kutumia fursa hiyo kujifunza namna nzuri ya kuboresha viwango vya bidhaa zao na kubadilishana ujuzi na uzoefu, kupanua masoko na kubaini teknolojia zitakazorahisisha uzalishaji wa bidhaa.

Awali, Waziri Mkuu alitembelea mabanda mbalimbali ya washiriki wa maonesho hayo yakiwemo ya taasisi za Serikali zinazotoa huduma katika sekta ya viwanda na biashara ambazo ni pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini  (TFDA) na  Wakala wa Vipimo Nchini (WMA).

Waziri Mkuu ametoa wito kwa taasisi hizo kuhakikishe zinafanya kazi kwa kushirikiana, ujuzi na weledi ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kuendesha shughuli zao kwa viwango vinavyotakiwa.