Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema manufaa mengi yanatarajiwa kupatikana iwapo Bunge litaridhia azimio la uendelezaji wa bandari ambalo litawezesha Serikali kuendelea na hatua zinazofuata za majadiliano na Serikali ya Dubai.
Baadhi ya manufaa yatakayopatikana ni kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 kwa sasa mpaka saa 24.
Hii itapunguza gharama za utumiaji wa bandari na matokeo yake itaongeza idadi ya meli zitakazokuja bandari ya Dar es Salaam kutoka 1,569 zilizohudumiwa mwaka 2021/22 mpaka kufikia takribani meli 2,950 ifikapo mwaka 2032/33.
Uwekezaji huo pia utapunguza muda wa ushushaji wa makontena kutoka siku 4.5 mpaka siku 2, kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka saa 12 mpaka saa moja kutokana na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA, pamoja na kuongezeka kwa mapato ya Serikali yatokanayo na Kodi ya Forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa bandarini kutoka shilingi Trilioni 7.76 za mwaka 2021/22 hadi
shilingi Trilioni 26.7 za mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 244.
Aidha, Watanzania wengi zaidi watapata ajira kutoka 28,990 mwaka 2021/22 hadi ajira 71,907 ifikapo mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 148 na shehena ya mizigo inayohudumiwa itaongezeka kutoka tani Milioni 18.41 za mwaka 2021/22 hadi kufikia tani Milioni 47.57 mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 158.
Mbali na bandari, ushirikiano huo utachochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi zikiwemo za kilimo, mifugo na uvuvi, kuchagiza shughuli za viwanda na biashara, kuchagiza ukuaji wa sekta ndogo za usafirishaji kwa njia ya reli (SGR, TAZARA na MGR) na barabara.
Pia, Watanzania watanufaika na teknolojia na ujuzi wa uendeshaji wa bandari kisasa; na kujenga mahusiano ya kidiplomasia.