Serikali yasema hakuna upungufu wa sukari nchini

0
1662

Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa hakuna upungufu wa sukari hivyo hawapaswi kuwa na wasiwasi wa aina yoyote ile.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya sukari.

Bashungwa amesema ni kweli bei ya sukari imepanda lakini haisababishwi na upungufu wa sukari bali imesababishwa na waagizaji kushindwa kuagiza kwa wakati kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unayosababishwa na kirusi cha Corona.

Ili kukabiliana na kadhia hiyo serikali imetoa vibali vya jumla ya tani 40,000 kwa kampuni nne za wazalishaji ambapo kila kampuni imeagiza tani 10,000.

Waziri Bashungwa amesema kuwa tayari sukari iliyokwisha ingia bandarini kupitia kampuni ya Kagera Sugar ni tani 9,990 na imeanza kutolea bandarini tangu jana jioni.

Kadhalika tarehe 24, 28 na 30 kampuni ya Mtibwa Sugar itaingiza jumla ya tani 10,000. Kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza jumla tani 1,624 hivi karibuni kutoka Malawi na Msumbiji huku tani 1,800 ikiagizwa kutoka Afrika Kusini.

Sambamba na hayo amesema kuwa wiki ya kwanza ya mwezi Mei Kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza tani 7,276 huku tarehe 15 Mei Kampuni ya TPC itaingiza tani 5,000 na tarehe 30 Mei Tani 4,500 zitaingia nchini.

Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amesema kuwa wizara inatarajia kuomba nyongeza ya tani 58,000 ili kukidhi mahitaji ya sukari kufikia Juni 2020