Wizara ya Viwanda na Biashara imeweka utaratibu maalumu utakaowawezesha Wafanyabiashara katika maeneo ya mipakani kutoa taarifa juu ya vikwazo, changamoto au kero za kibiashara hasa zile zisizokuwa za kikodi wanazokutana nazo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi Stella Manyanya imesema kuwa, lengo la kuweka utaratibu huo ni kuwawezesha Wafanyabiashara kupata huduma haraka kupitia Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali zinazotoa huduma mipakani.
Kwa kujibu wa taarifa hiyo, kwa kuanzia, Wizara ya Viwanda na Biashara imetoa anuani maalumu za barua pepe na namba za simu za Watendaji ambazo kila Mfanyabiashara anayepata vikwazo anaweza kutoa taarifa kupitia namba hizo.
Aidha, Wizara inawataka Wakuu wa Taasisi hizo walioko kwenye vituo vya mipakani kubandika orodha hiyo kwenye mbao za matangazo ili kurahisisha mawasiliano.
Vikwazo visivyokuwa vya kikodi ni pamoja na rushwa ya kifedha na isiyo ya kifedha, urasimu na kutotoa miongozo ya taratibu zinazohitajika, kukosa taarifa muhimu na kutojua fursa zilizopo.
Kwa upande wa Wizara ya Viwanda na Biashara, taarifa hizo zinapaswa kutumwa kwa Mratibu wa Vikwazo Visivyo vya Kiushuru ,-Aneth Simwela kupitia barua pepe tanzania@tradebarriers.org au simu namba +255622259341.
Kwa changamoto za masuala ya Viwanda na Masoko, Wafanyabiashara na Wadau wanaweza kuwasilisha changamoto zao kupitia barua pepe dawatilamsaada@mit.go.tz au kuwasiliana na Andrew Shirima wa Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia namba ya simu +255713500532.
