Serikali kuendelea kudhibiti uingizwaji wa bidhaa kutoka nje

0
3481

Serikali imesema kuwa, itaendelea kudhibiti uingizwaji wa bidhaa mbalimbali kutoka nje ili kulinda viwanda vya ndani.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo hii leo,
alipotembelea kiwanda cha maziwa cha Asas kilichopo mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Amesema kuwa, Serikali imedhamiria kukuza uchumi na kufikia uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025 kupitia sekta ya Viwanda.

Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa, Serikali inaamini kuwa uchumi wa Viwanda ukiimarika, uchumi utakuwa kwa kasi kubwa, na matokeo yake yataonekana wazi kwa kupanua wigo wa ajira, soko la huduma na shughuli nyingine za kiuchumi. 
 
Ameipongeza kampuni hiyo ya maziwa ya Asas, kwa kuwa ni miongoni mwa kampuni chache zilizoanza kutoa elimu kwa wafugaji juu ya namna bora ya ufugaji ikiwa ni pamoja na kufuata kanuni bora za ufugaji wa kisasa na kuwapa uhakika wa soko.
 
Amesema kuwa, Serikali inathamini uwekezaji uliofanywa na kampuni hiyo ya Asas kwa sababu imeitikia wito wa Serikali wa ujenzi wa uchumi kupitia sekta ya Viwanda.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha maziwa cha Asas, -Fuad Abri amesema kuwa, kiwanda hicho kina mpango wa kupanua uzalishaji, kwa kujenga kiwanda kingine cha kusindika maziwa katika wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya na kipo katika hatua za mwisho kukamilika.
 
Awali, Waziri Mkuu Majaliwa alizindua kiwanda cha maji cha Mkwawa kilichopo mjini Iringa na kusema kuwa, ujenzi wa kiwanda hicho ni njia ya uhakika ya kupunguza tatizo la ajira na kwamba Serikali itaendelea kuwashawishi Wawekezaji wa ndani na nje ili Wananchi wengi waweze kupata ajira.

Kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kuzalisha na kufanya biashara ya maji safi na salama, mpaka sasa kimeajiri Wafanyakazi 158 huku ajira zisizo rasmi zikiwa Elfu Tatu.