Mashindano ya mbio ya Selous (Selous Marathon) yanayofanyika kila mwezi wa nane tangu mwaka 2019, leo yamezindua bima ili kuhakikisha usalama kwa washiriki wa mbio hizo endapo watakutwa na janga lolote wakati wa mashindano.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Selous Marathon, Imani Kajura amesema wanahakikisha mbio hizo zinakuwa salama na hii ni kutokana na changamoto iliyotokea mwaka 2020 ambapo mmoja wa washiriki aliumia na hivyo kuwagharimu gharama za matibabu.
Bima hiyo inayotolewa kwa ushirikiano kati ya Selous Marathon, CRDB na Sanlam itapewa kwa kila atakayelipia gharama za kushiriki mbio hizo, amesema Maureen Majaliwa, Mkuu Kitengo cha Bima CRDB.
Bima zitazotolewa ni pamoja na bima ya maisha ambapo endapo mshiriki atafariki wakati wa mbio shilingi milioni tano zitatolewa.
Bima nyingine ni bima ya matibabu ambapo shilingi milioni 1 itatolewa endapo mshiriki ataumia, na shilingi milioni nne atapewa mshiriki atakayepata ulemavu wa kudumu wakati wa kushiriki mbio hizo.
Mbio hizo zitafanyika Agosti 2021 mkoani Morogoro ambapo pia zitahusisha mbio za kukimbia porini ni milimani (trail run).