Sekta ya uwekezaji yaendelea kukua

0
428

Waziri wa Fedha na Mipango  Dkt Philip Mpango amesema kuwa sekta ya uwekezaji nchini imeendelea kukua ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki kutokana na ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani.

Waziri Mpango ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akiwasilisha kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mapendekezo ya serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa pamoja na mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa  2019/2020.

Kwa mujibu wa Waziri Mpango, ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zimeonyesha kuwa Tanzania imevutia uwekezaji wenye thamani ya Dola Milioni 1,180 za Kimarekani ikifuatiwa na Uganda.

Mapendekezo ya serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/2020 yanatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa  Taifa wa miaka mitano kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara pamoja na uwekezaji.

Kikao hicho cha uwasilishaji kwa Wabunge mapendekezo ya serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa pamoja na mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa  2019/2020 kimefunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.