Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema maonesho ya 46 ya Biashara Kimataifa, maarufu Sabasaba yamevuta idadi kubwa ya washiriki.
Amesema idadi ya washiriki kwa mwaka huu ni mara mbili ya ile ya mwaka 2021, na kwamba kwa mwaka huu kampuni za kitanzania 3,200 zilishiriki, 225 kutoka nje ya nchi huku zaidi ya wananchi laki tatu wakitembelea maonesho hayo.
Akifunga maonoesho hayo yaliyoanza Juni 28 mwaka huu katika viwanja vya Sabasaba mkoani Dar es Salaam, Dkt. Mpango amesema kupata washiriki wengi ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na mataifa mengine baada ya kuathiriwa na janga la UVIKO-19.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kutoa unafuu wa kodi kwa wafanyabiashara, kuongeza bajeti katika sekta ya kilimo na kuziongezea uwezo bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga.
Ametoa wito kwa washiriki wa maonesho hayo ya 46 ya Biashara Kimataifa kuzingatia kanuni za ushindani katika soko ikiwa ni kuheshimu mikataba, kuzalisha bidhaa bora zenye viwango na kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye mahitaji makubwa nchini.
Amezitaja bidhaa hizo kuwa ni pamoja na sukari, mafuta ya kula, unga wa ngano, bati, nondo na saruji.
Maonesho ya 46 ya Biashara Kimataifa yalianza Juni 28 mwaka huu na kufunguliwa rasmi tarehe 3 mwezi huu na Katibu Mkuu Sekretarieti ya Soko Huru la Biashara Afrika Wamkele Mene.