Saba kizimbani kwa madai ya kuiibia TANESCO milioni 400

0
3456

Emmaule Samwel, TBC Dar es Salaam

Watu saba wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mkoani Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka matatu likiwemo ya kughushi nyaraka na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Washitakiwa hao wamefikishwa katika mahakama hiyo na kusomewa mashitaka yao na wakili wa Serikali Adolf Lema mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Augustina Mbando.

Katika shitaka la kwanza ambalo linamuhusu mshitakiwa wa kwanza Yusuph Nguruko, Wakili Lema amesema mtuhumiwa anadaiwa kughushi vocha ya malipo kwa niaba ya UVIKIUTA wakati akijua ni uongo, kosa ambalo anadaiwa kulitenda Julai 31, 2019.

Shitaka la pili ni la kuwasilisha nyaraka ya uongo katika ofisi za TANESCO zilizopo Ubungo ambapo inaelezwa kwa kujua na kwa nia ya kudanganya, mtuhumiwa alighushi vocha ya malipo kwenda benki ya CRDB kwa niaba ya kikundi cha VIKIUTA.

Shitaka la tatu linawahusu washitakiwa wote ambapo mshitakiwa wa kwanza hadi wa saba wanadaiwa kujipatia fedha zaidi ya shilingi milioni 400 kutoka TANESCO kwa udanganyifu wakisema kuwa wao ni kikundi cha VIKIUTA, kosa ambalo wanadaiwa kulitenda Novemba 11, 2020 maeneo ya Kinondoni.

Hata hivyo mahakama imeweka wazi masharti ya dhamana ambapo kila mshitakiwa ametakiwa kusaini hati yenye thamani ya shilingi milioni 30 huku wadhamini wakipewa sharti la kusaini hati yenye thamani ya milioni 20 kila mmoja.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Aznzerani Kulele, Zacharia Iddi, Mrisho Khalaf, Moshi Mkumba, Ruwaichi Micha na Somso Fundikira

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 9 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wamepelekwa gerezani baada ya kushindwa masharti ya dhamana.