Rais Samia awatumbua mabosi wa bandari

0
4796

Rais Samia Suluhu Hassan amevunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL).

Rais amechukua uamuzi huo leo asubuhi alipofanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam na kuzindua maboresho gati namba sifuri hadi saba.

Mbali na uamuzi huo amemuagiza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kuichukulia hatua bodi ya manunuzi kwa kutoa tenda ya ujenzi wa meli kwa kampuni isiyo na uwezo.

Rais amesema baada ya tenda hiyo kutolewa kwa kampuni ya YÜTEK kutoka nchini Uturuki aliunda timu maalum kwa ajili ya kujiridhisha na uwezo wa kampuni hiyo, ndipo ikabainika kwamba haihusiki na ujenzi wa meli bali ni madalali ambao baada ya kushinda tenda, huajiri kampuni nyingine kufanya kazi hiyo.

Tenda hiyo ilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 438.8 ambayo ililisainiwa jijini Mwanza Juni 2021 ambapo meli hizo za kampuni ya Meli Tanzania ilihusisha meli za mizigo na abiria.

Baada ya kutilia shaka tenda hiyo aliunda timu iliyokwenda Uturuki ambayo ilijumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Askari kutoka kikosi ya wanamaji cha JWTZ, na wataalamu kutoka MSCL.

Mbali na kuwa madalali, timu hiyo ilibaini kuwa YÜTEK haina na uwezo wa kifedha wala wataalamu kutekeleza mkataba huo.