Rais Magufuli apiga simu kumpongeza bilionea mpya wa Tanzanite

0
1027

Rais wa Tanzania, John Magufuli amempongeza mchimbaji mdogo Saniniu Laizer kufuatia kupata mawe mawili ya Tanzanite yenye thamani ya shilingi bilioni 7.8 ambayo ameiuzia serikali.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo wakati akizungumza kwa njia ya simu ya Waziri wa Madini, Doto Biteko ambaye ameongoza zoezi la serikali kukabidhiwa madini hayo.

“Nawapongeza sana wananchi wa Simanjiro kwa kazi nzuri wanazofanya kujitajirisha. Kwa sababu Tanzanite hii imekuwa ni kubwa sana haijawahi kupatikana mahali pengine, ndio maana namshukuru sana gavana pamoja serikali kwa kuamua kuinunua,” amesema Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Msanjila mawe hayo ambayo ni makubwa zaidi kuwahi kupatikana nchini yana jumla ya uzito wa 13.7kg, ambapo jiwe moja lina  9.2kg ambalo thamani yake ni shilingi bilioni 4.5 na la pili lina 5.8kg lenye thamani shilingi bilioni 3.3.