Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo amewahakikishia wafanyabiashara na wenye viwanda nchini kuwa nia ya Serikali ni kuona Viwanda na Biashara vinasimama vizuri, na vinaweza kushindana kimataifa lakini lengo ni kuwa vizalishe ili serikali nayo ipate kodi.
Prof. Mkumbo ameeleza hayo mkoani Arusha, wakati alipoambatana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti iliyoongozwa na Mwenyekiti wake Daniel Sillo kutembelea kiwanda cha nguo cha A to Z, ili kuangalia utekelezaji wa shughuli zake pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
“Niwahakikishie wafanyabiashara wote na wenye viwanda kuwa nia ya serikali ni kuona Viwanda vyetu na Biashara zetu zinasimama vizuri na zinaweza kushindana kimataifa lakini wakati huo huo lengo ni kuwa vizalishe kwa kiasi kikubwa ili Serikali nayo ipate kodi,” -amaeeleza Prof. Kitila Mkumbo
Prof. Mkumbo amesema kuwa Wizara ina mpango wa kuomba Bunge iridhie Tanzania kujiunga na mkataba wa biashara huru ukanda wa Afrika, ambapo viwanda vyetu hapa nchini vinahitaji kujipanga zaidi katika ushindani ndani ya Afrika na dunia kwa ujumla hivyo Tanzania ikisaini mkataba huo utasaidia kufungua masoko katika nchi 54 za Afrika.