Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ametoa nafasi kwa Wadau wa Utalii nchini kuwa Uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii upo tayari kupokea ushauri, mapendekezo pamoja na mawazo mapya yatayosaidia kuchochea na kuinua idadi ya watalii wa ndani.
Mhe, Kanyasu ametumia nafasi hiyo kwa kuwataka watu binafsi, mashirika pamoja na Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kutaka kuwekeza kwenye sekta ya utalii wasisite ofisi yake ipo wazi kwa mtu yeyote.
“Kwa yeyote atakayetaka kuniona kwa ajili ya kukuza na kuendeleza utalii hasa utalii wa ndani kwangu Mimi pamoja Waziri milango ipo wazi muda wote” alisisitiza Kanyasu.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Watalii wa ndani wapatao 200 kutoka jijini Dar es Salaam ambao walitembelea katika Msitu Asilia wa Magoroto katika wilaya ya Handeni mkoani Tanga kwa ajili ya kutalii ndani ya msitu wenye kila aina ya vivutio vya utalii likiwemo ziwa la kutengenezwa.
