MV Amani kuchochea biashara kati ya Tanzania na DR Congo

0
411

Wafanyabiashara mkoani Kigoma wametakiwa kutumia fursa ya kuanza kwa safari za meli ya MV Amani ambayo ni kubwa na ya kisasa katika Ziwa Tanganyika kuongeza kiwango cha mizigo ya kupelekwa DRC Congo bila kuhofia hatari ya kuzama kwa mizigo iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

Akizungumza wakati wa kuipokea meli hiyo ambayo imefika kwa mara ya kwanza katika safari ya majaribio, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema kwa muda mrefu wananchi wa Tanzania, wameshindwa kukuza biashara zao kutokana na ukosefu wa usafiri wa uhakika hivyo uwepo wa meli hiyo ni chachu kwa Watanzania kulitumia soko la Congo Mashariki lenye watu zaidi ya milioni 120.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa huo, Rashid Mchata amesema kufika kwa meli hiyo ni matokeo ya kongamano la biashara lililofanyika mwaka jana mkoani Kigoma na kukubaliana kuwepo kwa haja ya wafanyabiashara kusaidia juhudi za serikali katika kuhakikisha kunakuwepo vyombo vya usafiri vya uhakika baina ya Tanzania na DRC katika Ziwa Tanganyika.

Akitoa salamu za wafanyabishara wa DRC, Mkurugenzi Mkuu wa Amani International Business, Solomon Nasuma amesema wameamua meli hiyo ianze majaribio katika ardhi ya Tanzania kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za viongozi wa mataifa hayo mawili katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara.

Ameongeza kuwa meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 600, mizigo tani 3,500 na magari 50 kwa wakati mmoja na kuongeza kuwa uwepo wa meli hiyo ni chanzo cha ajira kwa wananchi wa Tanzani na kufungua ukurasa mpya wa kukuza uchumi wa watu wa Kigoma na kuboresha maisha yao.