Minada ya wazi ya mauzo ya Korosho kwa msimu wa mauzo wa 2019/2020, imeanza hii leo katika maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Wanunuzi watakaoshiriki katika minada hiyo ni wale ambao wamesajiliwa na kupatiwa leseni na Bodi hiyo.
Taarifa hiyo ya CBT imeongeza kuwa, Wanunuzi hao wa Korosho wanatakiwa kutumbukiza zabuni za kuomba kununua korosho kwenye sanduku lililowekwa katika eneo la mnada, zabuni zinazoonyesha jina la mnunuzi, bei na kiasi cha korosho kitakachonunuliwa.
Imefafanua kuwa, zabuni hizo zitakua zikipokelewa kuanzia saa Mbili asubuhi hadi saa Kumi jioni, na baadaye kufunguliwa katika eneo la mnada mbele ya Wakulima wa Korosho.
Mnunuzi atakayeruhusiwa kununua korosho hizo atatakiwa kuzilipia ndani ya kipindi cha Siku Nne, na Mkulima atapaswa kulipwa fedha zake ndani ya siku Kumi za kazi toka siku ya mauzo ya korosho hizo mnadani.
Kwa wiki ya kwanza, minada hiyo ya mauzo ya Korosho ambayo itakua ya Wazi itafanyika Oktoba 31 ambayo ni hii leo, Novemba Pili pamoja na Novemba Tatu mwaka huu katika maeneo ya Newala Mjini na Masasi mkoani Mtwara, pamoja na Kijiji cha Chiuta na Ruangwa Mjini mkoani Lindi.