Meneja wa TTCL atumbuliwa, Shirika la Posta kuchunguzwa

0
333

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew ametengua uteuzi wa Meneja wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) mkoa wa Kagera, Irene Shayo kuanzia Julai 30, 2021 kwa kile kilichobainika kuwa taratibu za uteuzi wake zilikiukwa na utumishi wake umekuwa wa kusuasua.

Shayo anasemekana kukwepa ziara za viongozi katika eneo lake pamoja na kupika taarifa za mapato na matumizi.

“Ninaagiza Meneja wa Mkoa wa Kagera aondoshwe mara moja katika Mkoa wa Kagera na kuanzia leo asitambulike kama Meneja wa Mkoa wa Kagera, taratibu zifuatwe na apangiwe kazi nyingine kulingana na wasifu wake kitaaluma ili aweze kufanya kazi vizuri kwasababu majukumu ya sasa hana uwezo nayo,” amesema Mathew.

Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo ametembelea na kukagua ukarabati wa Ofisi za Shirika la Posta Bukoba zilizogharimu kiasi cha shilingi milioni 78.8, na kueleza kutorudhishwa na kiasi cha fedha kilichotumika kwa sababu hakiendani na hali halisi ya ukarabati uliofanywa na kuagiza uchunguzi ufanyike ili kubaini gharama halisi zilizotumika katika ukarabati huo.

Mhandisi Mathew akasema, “Nimetoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali aunde kamati itakayohusisha wataalam wa ujenzi, TAKUKURU na Ofisi ya Usalama wa Taifa (W) ili wakafanye tathmini na kujiridhisha na kile ambacho kimefanyika.” Iwapo ikibainika kuna watu ambao wamefanya ubadhirifu wa fedha za umma watachukuliwa hatua za kisheria.

Sambamba na hilo ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, na Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta kuhakikisha mameneja wao wa Mikoa ambao hawana vigezo na uwezo wa kuongoza mikoa hasa ile ya kimkakati wanaondolewa na kuwekwa watu wenye uwezo na vigezo vya kuongoza katika mikoa hiyo.