Mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka 2021, umeongezeka hadi kufikia wastani wa asilimia 7.3 kutoka wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha mfano cha uchenjuaji wa madini cha Kantete wilayani Bukombe mkoani Geita akitoa ufafanuzi wa utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Kwa upande mwingine Biteko amesema sekta ya madini imefanikiwa kwa sababu za utoaji wa leseni za uchimbaji mkubwa kwa madini ya nikeli na dhahabu, sambamba na kusainiwa kwa mikataba ya madini ikiwemo ya graphite, madini mazito ya mchanga wa baharini.
Ameeleza kuwa jitihada hizo zitapelekwa kuanzishwa kwa migodi mikubwa na ya kati jambo ambalo litazidi kuongezea thamani madini, kukua kwa ajira, kukuza uchumi na kuongeza mchango wa sekta kwenye pato la taifa kufikia asilimia 10 ifikapo mwkka 2025.
“Sekta ya Madini imechangia asilimia 45.9 ya uuzaji wa bidhaa zote nje ya nchi na kuliingizia taifa dola za Marekani milioni 3,103.20 huku kasi ya ukuaji wa sekta mwaka 2021 imekuwa na kufikia asilimia 9.6 ikilinganishwa na asilimia 6.7 mwaka 2020 na kuwa ya tatu miongoni mwa sekta nyingine kutokana na ongezeko la uwekezaji nchini,” amesema Waziri Dkt Biteko