Mawakala wa utalii watembelea Mafia

0
2401

Mawakala wa utalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wapo katika kisiwa cha Mafia mkoani Pwani kwa lengo la kuangalia vivutio vya utalii vinavyopatikana katika kisiwa hicho.

Wakiwa katika kisiwa hicho cha Mafia, Mawakala hao pamoja na mambo mengine wataishauri Bodi ya Utalii Nchini (TTB)  namna ya  kuweka mpango maalumu wa kutangaza vivutio hivyo vya utalii  ambavyo baadhi yake  havipatikani mahali popote Barani Afrika isipokuwa  Mafia  pekee.

Mawakala hao wameyataja  maeneo ambayo yakitangazwa vizuri yanaweza kuvutia watalii wengi  kutembelea kisiwa cha Mafia kuwa ni ni pamoja na lile analopatikana samaki  mkubwa aina ya Potwe ambaye katika  Bara la Afrika hupatikana katika kisiwa hicho cha Mafia peke yake.

Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya bahari Dkt Jean de Villiers  amesema kuwa samaki aina ya Potwe ni kivutio kikubwa kinachopendwa  kuonwa na watalii wengi,  hivyo ni wajibu wa Bodi ya Utalii Nchini kuona kivutio hicho kama fursa pekee inayoweza kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea kisiwa cha Mafia na kuchangia pato la Taifa.

Kwa mujibu wa Bodi hiyo ya Utalii Nchini, mafanikio makubwa yanatarajiwa kupatikana baada ya Mawakala hao wa utalii kutoka mataifa mbalimbali duniani kutembelea maeneo matano makubwa yenye vivutio vikubwa vya utalii nchini kikiwemo  kisiwa cha Mafia  na Zanzibar.