Marufuku kufanya biashara kwenye basi bila barakoa

0
302

Na Sauda Shimbo

Jeshi la Polisi latatua changamoto ya wafanyabiashara ndogondogo ndani ya mabasi kipindi hiki cha UVIKO-19

MOSHI

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, limepiga marufuku wafanyabiashara wadogowadogo katika Stendi Kuu ya mabasi mjini Moshi kufanya biashara ndani ya mabasi bila kuvaa barakoa kwani kufanya hivyo ni ukiukwaji wa maagizo ya serikali.

Hayo yamesemwa mjini Moshi na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro Simon Maigwa wakati wa ukaguzi wa kuangalia namna ya abiria wanavyofuata maelekezo ya Wizara ya Afya ya kujikinga na ugonjwa wa uviko 19 ikiwemo uvaaji wa barakoa.

Kamanda Maigwa amesema amepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya abiria ya uwepo wa wafanyabiashara hao ambao wanauza bidhaa ndogondogo, ndani ya mabasi huku wakiwa hawana barakoa.

Amesema iwapo mfanyabiashara atakaidi agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Baadhi ya abiria wamesema mbali na kuvaa barakoa ni vyema serikali pia wangeweka utaratibu wa kuweka maji tiririka na sabuni katika mabasi mwanzo na mwisho wa safari ili waweze kunawa ikiwa ni mojawapo ya kinga ya ugonjwa wa Uviko 19.

Nao madereva wa mabasi yaendayo mikoani wameliomba jeshi la polisi kufanya ukaguzi wa uvaaji wa barakoa kwa abiria katika kila kituo cha ukaguzi cha jeshi hilo.