Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema ada ya maegesho ya magari katika maeneo yanayosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) zitaanza kulipwa kwa njia ya mtandao kuanzia Septemba Mosi mwaka huu.
Makalla amesema hayo alipokuwa akizindua mfumo wa kielektroniki utakaotumika kulipa ada hiyo badala ya malipo ya fedha taslimu yanayofanyika hivi sasa.
Amesema mfumo huo utasaidia kumaliza utapeli, kwa kuwa kumekuwa na watu ambao wamekuwa wakifanya udanganyifu kwenye makusanyo ya maegesho ya magari.
“Kumekuwa na watu hawapo TARURA, Jiji wala Manispaa lakini wameanzisha utaratibu wa kukusanya mapato ya maegesho yanayoishia kwenye kikundi cha watu, sasa mfumo huu ni mwarobaini wa vishoka wa maegesho ya magari.” amesema Makalla.
Kwa upande wake Stanley Mlula ambaye ni Mkuu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) – TARURA amesema, mfumo huo utaunganishwa na ule wa polisi unaosaidia kuwabaini wadeni.