Magazeti ya Nipashe na The Guardian yaonywa upotoshaji suala la Tanzania na Dubai

0
535

Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson ameyaonya magazeti ya Nipashe na The Guardian kwa kutoa taarifa zisizo sahihi kuwa Bunge limejadili na kupitisha makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai Kuhusu Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii kwa ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji Kazi katika Bandari Tanzania.

Spika Tulia ametoa onyo hilo leo bungeni jijini Dodoma akisema kuwa Bunge bado halijajadili suala hilo, na kwamba sasa mchakato upo kwenye kamati ambapo inaendelea kupokea maoni ya wadau na wananchi.

“Baada ya kamati kumaliza kazi zake, muswada huo umepangwa kuingia bungeni tarehe 10 Juni 2023 kwa ajili ya mjadala na kupitishwa na Bunge,” amesisitiza Spika.

Aidha, amewasihi waandishi wa habari kuhakikisha wanapata taarifa kutokana mamlaka husika kwani kitendo kilichofanywa na magezeti hayo ni kinyume na matakwa ya kanuni za bunge zinazoeleza kuwa “ni kosa kisheria kuchapisha habari za uongo au zinazolenga kwa namna yoyote kupotosha kwa makusudi jambo lolote linalohusu uendeshaji wa shughuli za bunge na kamati zake.

Amesema onyo hilo ni la mwisho na kwamba upotoshaji mwingine utakaofanywa na chombo cha habari utashughulikiwa kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu za bunge.

Spika Tulia ametumia jukwaa hilo kusisitiza kuwa Bunge litaendela kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi na maendeleo ya Watanzania.