Mafia yatakiwa kuandaa mazingira ya uwekezaji wa Utalii

0
3566

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula,  ameitaka halmashauri ya wilaya ya Mafia mkoani Pwani kuandaa mazingira ya  kupokeaWawekezaji katika sekta ya utalii kwa kupanga na kupima maeneo yake.

Dkt Mabula ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti, baada ya kusikiliza kero za migogoro ya ardhi kutoka kwa Wakazi wa kata za Baleni na Kilindoni, akiwa katika ziara yake ya siku mbili iliyokua na lengo la kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi, kukagua masijala ya ardhi pamoja na mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi kwa njia ya Kielektroniki.

Amesema kuwa,  eneo la Mafia limekaa kimkakati na yasipofanyika maandalizi mapema kama vile kupima maeneo ya Uwekezaji,  basi migogoro ya ardhi haitaisha na hivyo kuwafanya Wawekezaji kushindwa kuwekeza katika wilaya hiyo.

“ Huu ni mwaka wa uwekezaji, Wizara ya ardhi ni Wizara wezeshi,  tutafanya kila jitihada kupima viwanja katika eneo la Mafia, kwa kuwa watu wengi wanataka kuwekeza Mafia lakini Mafia yenyewe haijawa tayari” amesema Dkt Mabula.