Kioo miongoni mwa bidhaa zitakazotangulia AfCFTA

0
939

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amekishauri kiwanda cha Kioo Limited kuendelea kuzalisha bidhaa za kioo kwa wingi, zenye ubora na viwango vinavyohitajika kwa ajili ya soko la Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Aidha, amekishauri kiwanda hicho kuzalisha bidhaa za kioo zitakazotumika kama vifungashio kwa ajili ya wajasiriamali wadogo, ili waweze kuhimili ushindani katika biashara na kuweza kuingia katika soko la AfCFTA.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo alipotembelea kiwanda cha Kioo Limied kilichopo Chang’ombe, Dar es Salaam kwa lengo la kuangalia bidhaa za kioo zinazozalishwa na kiwanda hicho zinazotarajiwa kuingizwa katika soko la AfCFTA.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi nane za mwanzo zilizopewa kipaumbele cha kupeleka bidhaa kwenye soko hilo ambapo miongoni mwa bidhaa 10 zitakazotangulia kuingia katika soko hilo kuanzia Julai Mosi mwaka huu ni pamoja na Kahawa, Marumaru na kioo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda hicho Kumar Krishnan amesema, kiwanda cha Kioo kipo tayari kuingiza bidhaa ya kioo katika soko la AfCFTA kwa kuwa kina uwezo wa kuzalisha zaidi ya chupa milioni moja kwa siku ambazo huuzwa ndani na nje ya nchi.