Indonesia zaidi kuwekeza Zanzibar

0
569
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa Indonesia Nchini Tanzania, Prof. Ratlan Pardede, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.  Hussein Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka Indonesia kuwekeza Zanzibar kutokana na uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Indonesia nchini Profesa Ratlan Pardede, aliyefika Ikulu jijini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.

Amemueleza Balozi Pardede kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuimarisha uchumi wake, hivyo iko tayari kushirikiana na washirika wengine wa maendeleo ikiwemo Indonesia.

Rais Dkt. Mwinyi amefafanua kuwa, Zanzibar ina maeneo mengi ya kushirikiana na Indonesia hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa kiuchumi.

Naye Balozi Pardede amemuhakikishia Dkt. Mwinyi kuwa Indonesia itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake ikiwa ni pamoja na kuitangaza zaidi kwa wawekezaji wa nchi hiyo.

Amemuhakikishia Dkt. Mwinyi kuwa atahakikisha wawekezaji kutoka Indonesia wanawekeza katika miradi iliyopo Zanzibar ukiwemo ule wa bandari kuu ya Mangapwani – Bumbwini mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu.