IMF kuipatia Tanzania mkopo wa trilioni 1.3

0
5851

 
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeridhia kutoa mkopo nafuu kwa Tanzania wa dola milioni 567.25 za Kimarekani sawa na shilingi trilioni 1.3, kwa ajili ya kukabiliana na athari za UVIKO -19.
 
Fedha hizo zinajumuisha mkopo nafuu usio na riba wa jumla ya dola milioni 189.08 za kimarekani,  na mkopo nafuu wenye riba ndogo wa dola milioni 378.17 za kimarekani.
 
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na wizara ya Fedha na Mipango imeeleza kuwa,  fedha hizo zitatumika ndani ya mwaka huu wa fedha katika kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na UVIKO -19.
 
Sekta zitakazonufaika kulingana na makubaliano ya Tanzania na IMF ni afya, elimu, utalii, maji, pamoja na kusaidia kaya maskini kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (TASAF) na kuwezesha makundi maalum ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.
 
Kila sekta itatumia fedha hizo kwenye masuala yanayolenga kukabiliana na athari za UVIKO -19 ambapo pamoja na mambo mengine sekta ya afya itanunua dawa na vifaa tiba vya kupambana na UVIKO -19 na kugharamia utekelezaji wa mpango wa chanjo.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya wizara ya Fedha na Mipango, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itawezeshwa ili iweze kukabiliana na athari za UVIKO -19 katika sekta zilizoathirika ikiwa ni pamoja na afya, utalii na kilimo.
 
Waziri Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka sekta zote zitakazopata fedha hizo kuzitumia kulingana na mpango ulioandaliwa na pia zitumike kwa kuzingatia makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Shirika hilo la Fedha la Kimataifa.