Ghana yahofia vitisho vya EU

0
261

Serikali ya Ghana imepiga marufuku usafirishaji wa mboja za aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na bilinganya na pilipili  kutoka nchini humo kwenda nchi za nje,  kwa hofu kuwa zinaweza zikawa na wadudu waharibifu wa mazao.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Chakula na Kilimo ya Ghana imesema kuwa, utekelezaji wa  marufuku hiyo unaanza wiki ijayo na haijulikani itamalizika lini.

Uamuzi huo wa Serikali ya Ghana wa kupiga marufuku usafirishaji wa mboja za aina mbalimbali kutoka nchini humo kwenda nchi za nje, unafuatia maelekezo yaliyotolewa na Umoja wa Ulaya (EU) yanayozitaka nchi zote kuandaa taarifa ya namna zinavyokabiliana na wadudu waharibifu wa mazao.

Kufuatia uamuzi huo wa Serikali ya Ghana, Umoja wa Wakulima na Wasafirishaji wa mboga nchini humo, umeiomba serikali kuahirisha mafuruku hiyo kwa kuwa utekelezaji wake utawaathiri takribani wakulima Elfu Nne wa mboga.

Hata hivyo Serikali ya Ghana imesisitiza utekelezaji wa marufuku hiyo ya usafirishaji wa mboja za aina mbalimbali kutoka nchini humo kwenda nchi za nje, ili kuepuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya endapo itashindwa kuandaa taarifa ya namna inavyokabiliana na wadudu waharibifu wa mazao.