Geita kuwa kitovu cha biashara

0
1911

Rais Samia Suluhu Hassan amesema fursa na miundombinu inayoendelea kutengenezwa katika mkoa wa Geita inakwenda kuupa hadhi mkoa huo na kuufanya kuwa kitovu cha uchumi kwa kutumia fursa zilizopo kupitia mwambao wa Ziwa Victoria, madini na viwanda vya kusafisha na kuongeza thamani ya madini ya dhahabu

Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kalangalala mkoani humo.

Aidha, amewaagiza viongozi wa wizara ya madini kuangalia upya tozo zilizopo kwenye sekta ya madini na kuendelea kuwapa unafuu wachimbaji wadogo na wawekezaji wa ndani ili kunufaika na shughuli za uwekezaji ndani ya nchi yao

Rais Samia amewashukuru wananchi wa Geita kwa kuendelea kujitokeza kwa wingi na kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha kaulimbiu ya Kazi Iendelee na kujiletea maendeo ya mtu binafsi na Taifa zima.

Kwa upande wake Waziri wa TAMISEMI, Angellah Kairuki amesema serikali itaendelea kuhakikisha inajenga miundombinu imara ya elimu na afya, kugawa magari ya wagonjwa  na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.

Geita inaenda kuunganishwa na nchi nyingine kupitia daraja la Busisi-Kigongo na kuongeza fursa katika masuala ya uchumi, biashara na fursa za maendeleo kwa wananchi wa Geita na mikoa jirani.