DART yaingiza barabarani mabasi mapya

0
2582

Mabasi mapya 70 ya mwendokasi yaliyoachiwa na serikali hivi karibuni yameanza kutoa huduma na hivyo kufanya jumla ya mabasi yanayotoa huduma kufikia 210.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Wakala ya Mabasi yaendayo Haraka (DART), Philemon Mzee jijini Dar es Salaam ambapo ameeleza kuwa utaratibu wa manunuzi wa mabasi mengine ili kufikisha jumla ya mabasi 305 yanayohitajika unaendelea.

Mabasi hayo yalichelewa kuanza kutoa huduma kutokana na kushikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tangu mwaka 2018 kutokana na kutolipiwa kodi ili yaweze kutoka bandarini.

“Kwa sasa tunaendelea na utaratibu wa kuhakikisha mabasi yote yanafanya kazi ikiwemo yale yaliyokuwa mabovu yaliyokuwa yamesimama bila kutoa huduma,” amesema Mzee.

Ujenzi wa awamu ya pili ya mradi huo kutoka Kariakoo hadi Mbagala unaendelea ambapo ujenzi wa vituo vya mlisho unatarajiwa kukamilika mwezi huu, huku ujenzi wa barabara ukitarajiwa kukamilika Machi 2023.

Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara katika kituo cha Gerezani na kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa DART, Suzan Chaula kwa kutoridhishwa na utendaji kazi wake.