Benki ya Afrika (BOA) Tawi la Tanzania, imeongezewa mtaji wa Shilingi Bilioni 22.9 na Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo, ili kuwawezesha Wateja wake kuendelea kupata huduma bora.
Uamuzi wa bodi hiyo umefanyika katika kikao chake kilichofanyika mjini Madrid nchini Hispania, na kwamba pesa hizo zitaongeza nguvu katika mkakati wa benki hiyo wa kuwafikia Wajasiriamali wengi zaidi hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo ya Afrika Tawi la Tanzania,- Joseph Iha amewaambia Waandishi wa habari jijini Dar es salaama kuwa, fedha hizo zinawaongezea uwezo wa kuwahudumia Wajasiriamali wengi zaidi ambapo mpaka sasa wameishawafikia Wajasiriamali Elfu Tisa ambao wamepewa mtaji wa zaidi ya Shilingi Bilioni 27.
Ameongeza kuwa fedha zilizotolewa na Bodi pamoja na Wanahisa wa benki hiyo ya Afrika, zitasaidia kuboresha huduma za benki hiyo na kuwafikia Wajasiriamali wengi katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.