Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini Dkt. Benson Ndiege amewasihi Vijana nchini kujiunga na Benki ya Taifa ya Ushirika (NCB) kwani ni uwekezaji mzuri kuuanza katika umri mdogo.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati wa mdahalo wa uanziishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika huko mkoani Kilimanjaro, Dkt. Ndiege amesema dhana kuwa vyama vya ushirika ni vya wazee zaidi si njema kwani vyama hivyo ni vya vijana pia.
“Mwalimu wangu kwenye kazi aliniambia Wajapani wanasema ili kuwa na ushirika imara lazima mtu kuanza kuwa mwanaushirika akiwa mtoto.” ameeleza Dkt. Ndiege na kuongeza kuwa
“Ushirika mwingi wa Tanzania tunaukuta wakati ule tunapoanza kulima korosho, tunapoanza kufanya biashara za Mamantilie…mwisho wa siku wanakuwa ni wanaushirika ambao sio waumini wa ushirika lakini kwa sababu mfumo unawataka wawe wanaushirika.”
Katika mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 yaliyowasililishwa bungeni jijini Dodoma katika Bunge la bajeti linaloendelea hivi sasa, vyama vya akiba na mikopo vimeagizwa kutenga asilimia 5 ya mtaji wao kwa ajili ya uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika.
Dkt. Ndiege ametoa wito kwa Watanzania wa rika zote wakiwemo Wanafunzi ambao wameshiriki mdahalo huo kuwekeza NCB, kwani ni uwekezaji wa muda mrefu na utawanufaisha katika miaka ijayo.
Pia amewataka Viongozi wa vyama vya ushirika nchini kuwaelimisha Vijana kuhusu namna wanavyoweza kuwa Wanachama wa benki hiyo pamoja na bei za hisa ili wawe mstari wa mbele katika kuwekeza na kufaidika.
Baadhi ya vigezo vya kujiunga na vyama vya ushirika pamoja na benki hiyo ya NCB ni mtu kuwa na umri wa kuanzia miaka 18 pamoja na akili timamu.
Kingine ni awe anajishugulisha na shughuli ama kazi inayohusika na chama cha ushirika anachotaka kujiunga nacho.