Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imezitoza faini Benki Tano za Biashara kwa kukiuka kanuni namba 17, 22 na 28 za kanuni za kuzuia utakatishwaji Fedha za mwaka 2012.
Benki hizo pia zimetozwa faini kwa kushindwa kuhakiki taarifa za utambulisho wa Wateja na kushindwa kuwasilisha taarifa ya miamala yenye kuleta mashaka katika Kitengo cha Kuzuia Fedha Haramu (FIU).
Benki hizo ni African Banking Corporation (T) Limited iliyotozwa faini ya Shilingi Milioni 145, Equity Bank Tanzania Limited Shilingi Milioni 580 na I&M Bank (T) Limited Shilingi Milioni 655.
Nyingine ni UBL Bank (T) Limited ambayo imetozwa faini ya Shilingi Milioni 325 na Habib African Bank Limited faini ya Shilingi Milioni 175.
Aidha, Benki Kuu ya Tanzania imezitaka benki hizo kupitia upya taarifa za Wateja wao na kuhakikisha zinakidhi matakwa ya kisheria na kanuni zilizopo za uhakiki wa utambulisho.
Pia zimetakiwa kuwasilisha taarifa ya miamala yenye kuleta mashaka iliyotakiwa kuwasilishwa FIU na kufanya tathmini ya ubora wa mifumo ya ndani ya kibenki na kuchukua hatua stahiki.