Bei mpya za ukomo wa mafuta kwa mwezi Septemba zimeanza kutumika hii leo.
Bei hizo mpya za mafuta zimetangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na zimepungua baada ya kupanda mfululizo kwa miezi mitano kuanzia mwezi Aprili mwaka huu.
Kuanzia hii leo petroli imeanza kuuzwa kwa shilingi 2,969 kwa lita, dizeli shilingi 3, 125 na mafuta ya taa shilingi 3,335 kwa lita kwa mkoa wa Dar es Salaam baada ya ruzuku ya serikali.
Mpaka jana, kwa mkoa wa Dar es Salaam petroli iliuzwa kwa shilingi 3, 410 kwa lita, dizeli shilingi 3, 322 na mafuta ya taa yaliuzwa shilingi 3,765 kwa lita.
Kwa mujibu wa EWURA, kushuka kwa bei za mafuta nchini kumetokana na kupungua kwa bei za mafuta katika soko la dunia kwa mwezi Julai mwaka huu, ambapo mafuta yanayotumika kuanzia leo yamenunuliwa mwezi huo.