AfDB yaomba kuongezewa mtaji

0
520

Tanzania imeunga mkono uamuzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wa kutaka kuongezewa mtaji ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa mikopo kwa nchi wanachama wa benki hiyo kwa lengo la kuchochea zaidi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano wa Saba  wa Magavana  ambao ni Mawaziri wa Fedha kutoka nchi 54  wanachama wa Benki hiyo Mjini Washington nchini  Marekani, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango  ameeleza kuwa AfDB imefanya mambo makubwa nchini Tanzania,  ndio sababu inaunga mkono kusudio hilo.

Amesema kuwa Benki hiyo imeipatia Tanzania Mabilioni ya Shilingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, kilimo, nishati na maji.

AfDB inataka kuongezewa mtaji kwa asilimia 200 kutoka Dola  Bilioni 94.76  za Kimarekani hadi Dola Bilioni  268.6 za Kimarekani  ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na  ya kijamii ya nchi wanachama hususan katika ujenzi wa reli, barabara, usafiri wa anga, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), bandari, uzalishaji na usambazaji wa nishati.

“Wakati umefika ili twende haraka zaidi, mitaji sehemu nyingine imepungua, pendekezo la kuongeza mtaji wa benki hii ni jema na matokeo ya miradi inayofadhiliwa na Benki hii yanaonekana katika nchi zetu za kiafrika kwa sababu benki hii iko Afrika na inaijua Afrika tofauti na benki nyingine” amesisitiza Dkt Mpango.

Uamuzi wa nchi za Kiafrika zenye hisa katika Benki ya Maendeleo ya Afrika wa kutaka Benki hiyo iongezewe mtaji ulitolewa wakati wa mkutano wa Magavana wa Benki hiyo mjini Rome nchini Italia baada ya mahitaji ya nchi wanachama ya kutafuta mikopo kwenye taasisi hiyo kuongezeka.