Huduma za kibingwa za Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) zimeanza kutolewa katika hospitali mpya na ya kisasa ya rufaa kanda ya Kusini iliyopo mkoani Mtwara, ambapo mgonjwa wa kwanza amefanyiwa upasuaji.
Upasuaji huo wa kibingwa wa mifupa umefanywa na jopo la madaktari bingwa, wauguzi na wataalam wa usingizi kutoka MOI kwa kushirikiana na wataalam wa hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini.
Kiongozi wa jopo la wataalam kutoka MOI Dkt. Albert Ulimali amesema, jopo la wataalam 11 limepiga kambi ya siku tano katika hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu ikiwa ni pamoja na kuwafanyia upasuaji wagonjwa.
Daktari bingwa wa Mifupa kutoka MOI, Dkt Tumaini Minja amesema upasuaji wa kwanza katika hospitali hiyo umekuwa na mafanikio makubwa.
Amesema huduma hizo zitaendelea kupatikana hospitalini hapo, hivyo wakazi wa mikoa ya kusini wajitokeze kupata huduma.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo ya Rufaa Kanda ya Kusini Dkt. Jeofrey Ngomio ameishukuru Taasisi ya MOI kwa kusogeza huduma za kibingwa kwa wakazi wa mikoa ya kusini ambapo wagonjwa hawatalazimika kufuata huduma hizo mkoani Dar es Salaam.