Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga kimeeleza kutoridhirishwa na kasi ya ujenzi wa vituo vya afya katika kata za Mnyuzi na Kerenge vilivyopo wilayani Korogwe ambavyo licha ya Serikali kutoa fedha, ujenzi bado haujakamilika.
Akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa kituo cha afya kilichopo kijiji cha Mkwakwani kata ya Mnyuzi, Mganga mkuu wa wilaya ya Korogwe Dkt. Mariam Cheche amesema awamu ya kwanza kwa mwaka 2020/2021 Serikali ilitoa shilingi Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Mnyuzi ambapo kilikuwa kinatakiwa kijengwe majengo ya OPD, maabara na kichomea taka.
Mwaka 2022/2023 Serikali ilitoa tena shilingi Milioni 250 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi ambao mpaka sasa jengo la Mama na Mtoto linaendelea na kazi mbalimbali, huku kichomea taka kikiwa hakijajengwa na fedha haikutosha.
Kufuatia hali hiyo CCM mkoa wa Tanga imemuagiza Mkuu wa wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo kufuatilia kwa karibu miradi ya vituo hivyo ili kuhakikisha vinakamilika kwa wakati na kutoa huduma stahiki kwa Wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara yake wilayani Korogwe iliyokuwa na lengo la kuona uhai wa chama na kukagua shughuli za maendeleo, Mwenyekiti wa CCM mkoa Tanga Rajab Abrahaman Abdallah ametaka hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote waliohusika na ucheleweshaji wa ujenzi vituo hivyo ambavyo Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo.