Bohari ya Dawa (MSD) imefikia asilimia 95 ya usambazaji wa dawa na vifaa tiba wilayani Kyela mkoani Mbeya.
MSD imefanya hivyo pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali ambapo katika kijiji cha Ikombe kilichopo pembezoni mwa Ziwa Nyasa dawa zimefikishwa licha ya kijiji hicho kutokuwa na barabara.
Akizungumza na TBCOnline Mfamasia wa wilaya ya Kyela, Emannuel Chacha amesema, wamefanikiwa kufikikisha dawa katika kijiji hicho cha Ikombe kwa kutumia mitumbwi.
“Tuna vituo 37 vinavyopata dawa na vifaa tiba kwa mfumo wa kielektroniki wa ELMIS, kati ya vituo hivyo vyote vinafikika kasoro kimoja ambacho kipo kisiwani katika kijiji cha Ikombe kilichozungukwa na Ziwa Nyasa,” amesema Chacha.
Ameishukuru Serikali kwa kutoa kipaumbele kwa sekta ya afya na kuongeza kuwa hatua hiyo ni matokeo ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vyenye ubora na kwa wakati .
Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ikombe Dkt.Joshua Katabazi amesema,, ufikishaji wa dawa katika zahanati hiyo umekuwa na changamoto kutokana na kukosekana kwa barabara na kijiji kuzungukwa na Ziwa Nyasa.