Vijana Sitini wa Kitanzania wamewasili nchini Israel kwa ajili ya kushiriki mafunzo ya Kilimo kwa kipindi cha mwaka mmoja, huku wengine Arobaini wakitarajiwa kuwasili Septemba 11 mwaka huu kukamilisha idadi ya vijana Mia Moja.
Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Ben Gurion jijini Tel Aviv, vijana hao wamepokelewa na Waziri wa Kilimo wa Tanzania, – Japhet Hasunga.
Akizungumza na vijana hao, Waziri Hasunga amewataka kutumia mafunzo hayo kama chachu ya kuendeleza sekta ya kilimo pindi watakaporejea nchini.
“Ninyi mmekuja Israel mkiwa katika mtazamo wa kujifunza, hivyo mambo mengine yote wekeni pembeni mzingatie masomo na katika kipindi cha mwaka mmoja mhakikishe mmetumia muda wenu wa masomo vizuri kujifunza, kupata maarifa na ujuzi ili mtakaporejea nyumbani mlete mabadiliko makubwa kwenye kilimo”, amesema Waziri Hasunga.
Pia amewataka kuwa waaminifu wakati wote wa masomo yao, kwa kuwa wanaiwakilisha Tanzania, hivyo vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu itakuwa ni sehemu ya kulidhalilisha Taifa.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Israel, – Job Masima amewataka vijana hao kutekeleza maelekezo waliyopatiwa na Waziri huyo wa Kilimo.
“Chochote mtakachofanya ni Mtanzania amefanya, kwa hiyo mkifanya mabaya mtasambaza sifa mbaya ya nchi katika Mataifa mengine jambo ambalo halitakiwi”, amesisitiza Balozi Masima.