Dunia yamuaga Koffi Annan

0
2046

Viongozi mbali mbali duniani leo Alhamisi wameungana na familia ya Koffi Annan, wakati shughuli za mazishi ya Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa zikiendelea, katika nchi yake ya asili, Ghana.

Mamia ya waheshimiwa, wengi wao wakiwa wamevalia suti nyeusi zinazoashiria maombolezo, wamekusanyika katika kituo cha mikutano ya kimataifa jijini Accra, kuhitimisha siku tatu za maombolezo ya kitaifa (Ghana) kwa mwanadiplomasia aliyekuwa na heshima kubwa wakati wa uhai wake, Annan.

Viongozi hao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa sasa, Antonio Guterres, ambaye aliongoza waombolezaji wote kutoka ‘ulimwengu’ wa kidiplomasia, huku kukiwa na wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika (AU), Jumuia ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), na marais wengi kutoka bara la Afrika na nje ya Afrika.

Falme pia zilikuwepo, akiwemo ‘Princess’ Beatrix, malkia wa zamani wa Netherlands, aliyeongozana na mkwewe, Malkia Mabel, watu ambao walikuwa ni marafiki wa karibu wa marehemu Annan.

Annan aliongoza Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 1997 hadi 2006 akiwa ni mtu wa kwanza kutoka kusini mwa Sahara mwa bara la Afrika, kushika wadhifa huo.

Alikufa nyumbani kwake huko Switzerland Agosti 18 mwaka huu akiwa na umri wa miaka 80, baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Imeelezwa kuwa kabla ya mwili wa Annan haujazikwa, leo atapata heshima ya kupigiwa mizinga 17.