Serikali imesema kuwa itaendelea kuboresha huduma za mawasiliano katika maeneo mbalimbali hapa nchini na hasa vijijini, ili kuwawezesha Wananchi kupata huduma hizo na kurahisisha shughuli zao.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Elias Kwandikwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Same Mashariki Dkt Mathayo David aliyetaka kujua ni lini serikali itapeleka mawasiliano katika vijiji vilivyopo katika jimbo lake.
Baada ya majibu hayo, Wabunge wa maeneo mbalimbali walisimama na kutaka kufahamu ni hatua gani serikali inachukua kuboresha mawasiliano katika maeneo yao na hasa maeneo ya pembezoni.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Kwandikwa amesema kuwa serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote inafanya jitihada za kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na huduma za mawasiliano ya simu za mkononi.
Mhandisi Kwandikwa amesema kuwa hadi sasa zaidi ya vijiji Elfu saba vimefikiwa na mawasiliano ya simu za mkononi hapa nchini na kuahidi kuwa serikali itaendelea kupeleka huduma hiyo katika maeneo ambayo bado hayana mawasiliano.
Aidha ameongeza kuwa, ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali bado unaendelea ikiwa ni jitihada za serikali kuhakikisha inawapatiwa mawasiliano wananchi wake.