JPM awataka Wahandisi kufikiria kujenga kiwanda

0
155

Rais John Magufuli amewataka Wahandisi nchini kufikiria namna ya kuanzisha kiwanda ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za serikali za ujenzi wa viwanda hapa nchini.

Rais Magufuli amewataka Wahandisi kuungana na kujenga kiwanda hata kimoja kwa kuwa utalaamu wa kufanya hivyo wanao na uwezo wa kujenga kiwanda hicho pia wanao.

Rais Magufuli ametoa wito huo jijini Dar es salaam, wakati akifungua mkutano wa mashauriano baina ya Bodi ya Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Bodi ya Makandarasi (CRB) na Bodi ya Wahandisi (ERB).

“Niwaulize nyie Wahandisi, hamjawahi kufikiria kujenga kiwanda?, Wataalamu wa kujenga mnao, sasa kwanini hamjengi hata kiwanda cha kubangua korosho?, ama hata kiwanda cha kuchambua Pamba”, amehoji Rais Magufuli.

“Mbona hamjawahi kuomba hata mgodi wa chuma ili mchimbe chuma na hatimaye mzalishe vifaa vya ujenzi?, kaeni chini mfikirire nje ya boksi na muweze kutumia ujuzi wenu katika ujenzi wa viwanda”, amesisitiza Rais Magufuli.

Kuhusu vitendo vya rushwa katika zabuni mbalimbali, Rais Magufuli amewataka Makandarasi kuacha tabia ya kuwashawishi Watendaji wa serikali ili wapate zabuni na hivyo hivyo kuwataka watendaji wa umma kuacha kuomba rushwa kwa Makandarasi.

Aidha Rais Magufuli amewataka Makandarasi Wazalendo kuacha kulalamika kila mara na badala yake kuchangamka na kuomba zabuni za miradi mbalimbali ya maendeleo zinazotangazwa na serikali.

Amezitaka bodi zote Tatu ambazo ni AQRB, CRB na ERB kusimamia sheria na kuhakikisha miradi yote isiyozidi Shilingi Bilioni Kumi wanapewa Makandarasi wazawa na si vinginevyo.

Mkutano huo wa mwaka wa mashauriano wa Bodi Tatu za Kihandisi unafanyika kwa muda wa siku Mbili ambapo pia kuna maonesho ya shughuli mbalimbali za Kihandisi