Serikali imesema kuwa haijavunja mkataba wowote na wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu bali makato ya asilimia 15 kutoka kwenye mshahara ghafi wa mnufaika wa mkopo huo ni ya kisheria.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa bungeni, jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbozi,- Paschal Haonga juu ya kinachodaiwa kuwa serikali imevunja mkataba kinyume na makubaliano kwa kuwa wakopaji walisaini mkataba wa asilimia Nane na siyo 15.
“Kilichofanyika mwaka 2016 katika marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo (SURA 178) ni kuiboresha sheria hii kwa kutaja kiwango mahsusi cha asilimia 15 kinachopaswa kukatwa kutoka mshahara ghafi wa mnufaika. Awali, kabla ya marekebisho hayo, kifungu cha 7(1) (h), kiliipa Serikali mamlaka ya kupanga kiwango cha makato na kubadilisha kiwango pale itakapoona inafaa,” amefafanua Profesa Ndalichako.
Ameongeza kuwa serikali inafahamu umuhimu wa kuwashirikisha wadau katika marekebisho ya sheria yoyote, hivyo katika mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (SURA 178) ya mwaka 2016, wadau mbalimbali walishirikishwa.
Amewataja wadau walioshirikishwa kuwa ni pamoja na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi TUGHE na TUCTA, Chama cha Mawakili nchini (TLS) pamoja na wanafunzi kutoka Taasisi za Elimu ya Juu kama vile Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Elimu ya Biashara – Dodoma na Chuo cha Mipango.
Aidha Profesa Ndalichako amesema kuwa makato hayo ya asilimia 15 yana lengo la kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali zinarejeshwa kwa wakati ili ziweze kuwasomesha Watanzania wengine wahitaji.
Ametoa wito kwa wanufaika wote wa mikopo ya Elimu ya Juu kuhakikisha kuwa wanarejesha kwa wakati mikopo waliyokopeshwa na Bodi hiyo ili iweze kusaidia watoto wengine wenye uhitaji.