Mwelekeo wa mvua za Vuli

0
163

Taasisi mbalimbali nchini zimetakiwa kuchukua tahadhari mapema ili kukabiliana na athari za mvua zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwanzoni mwa mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka huu katika baadhi ya maeneo nchini.

Tahadhari hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt Agnes Kijazi na kusema kuwa hatua zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha athari mbalimbali zinazotokana na mvua hizo zinaepukika.

Dkt Kijazi amewaambia Waandishi wa habari kuwa, maeneo yanayozunguka Ukanda wa Ziwa Viktoria ambayo ni mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara, yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani kuanzia wiki ya Pili ya mwezi Oktoba.

Ameyataja maeneo mengine yaliyosalia ambayo ni Pwani ya Kaskazini pamoja na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki kuwa mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.

Dkt Kijazi ameongeza kuwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua nyingi, magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uhaba wa maji safi na salama na katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani unaweza ukajitokeza upungufu wa maji na malisho ya mifugo, hali inayoweza kusababisha migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji, hivyo ni vema tahadhari ikachukuliwa.

Kwa upande wa Pwani ya Kaskazini ambayo ina mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Tanga, Visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na maeneo ya Kaskazini ya mkoa wa Morogoro, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya Pili ya mwezi Oktoba ingawa mtawanyiko wake unatarajiwa kuwa hafifu.