Baziga auawa kwa kupigwa risasi Maputo

0
284

Kiongozi wa Raia wa Rwanda wanaoishi nchini Msumbiji, – Louis Baziga ameuawa kwa kupigwa risasi katika mji wa Maputo.

Habari kutoka nchini Msumbiji zinasema kuwa, Baziga alipigwa risasi akiwa kwenye gari yake wakati anatoka nyumbani kwake.

Kwa muda mrefu Baziga ambaye ni mfanyabishara mkubwa  na ambaye amekua akimiliki maduka mengi ya bidhaa pamoja na dawa nchini Msumbiji, amekua akitoa msaada mkubwa kwa serikali ya Rwanda inayoongozwa na Rais Paul Kagame.

Balozi wa Rwanda nchini Msumbiji, – Claude Nikobisanzwe amesema kuwa, baada ya kumfyatulia risasi Baziga, watu hao wenye silaha walikimbia bila ya kuchukua chochote na bado hawajapatikana.

Mfanyabishara huyo maarufu Baziga ameishi nchini Msumbiji tangu kutokea kwa mauaji ya halaiki ya nchini Rwanda na kwa sasa alikua ndiye kiongozi wa Raia wa Rwanda wanaoishi nchini Msumbiji.

Zaidi ya raia Elfu Tano wa Rwanda wanaishi nchini Msumbiji huku wakifanya shughuli mbalimbali.