Katuni inayomkejeli Serena yazua zogo

0
2132

Umoja wa kitaifa wa waandishi wa habari weusi nchini Marekani umeilaani vikali katuni iliyochapwa na gazeti la Herald Sun la Australia jana Jumatatu, iliyomchora katika namna ya kuchekesha mcheza tennis nyota duniani, Serena Williams, alipokuwa akimshambulia kwa maneno ‘umpire’ Carlos Ramos, katika mchezo wake na Naomi Osaka, Jumamosi iliyopita.

Umoja huo umesema katuni hiyo imebeba ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa kijinsia dhidi ya wanawake (sexism), tuhuma ambazo pia zilitamkwa na Serena wakati akimshambulia Ramos.

Katuni huyo imemchora Serena akiwa na umbo linalochekesha, huku akiruka ruka karibu na ‘racket’ iliyovunjika, ambapo pia mdomo wake ulikuwa umekuzwa na kuwa mkubwa na pua yake ikifanana na michoro iliyokuwa ikiwabagua watu weusi nchini marekani miaka ya zamani.

Mpinzani wa Serena katika mchezo huo Naomi Osaka amechorwa akiwa mwembamba kupita kiasi na akimsikiliza Ramos anayemwambia “kwa nini usimwachie ashinde tu?”

Katuni hiyo ‘imeshambuliwa’ huko Marekani baada ya baadhi ya watu nchini Australia kuisambaza katika mitandao ya jamii. Imeelezwa kuwa washabiki wa Serena walioko nchini Australia pia wameilaani vikali katuni hiyo.

Hata hivyo katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne, gazeti la Herald sun limesema kuwa katuni hiyo haikubeba dhana zozote za ubaguzi wa rangi wala jinsia.