Serikali imeagiza kaya 13 zilizopo eneo la Wafugaji katika hifadhi ya Wembele wilayani Igunga mkoani Tabora, kuondoka katika eneo hilo.
Agizo hilo la serikali limetolewa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa mkutano wake na Wakulima pamoja na Wafugaji katika eneo hilo.
Amezitaka kaya hizo kwenda eneo lililopangwa kwa ajili ya Wakulima ili kuondoa mgogoro wa muda mrefu kati ya Wakulima na Wafugaji.
Kauli hiyo ya serikali inafuatia Wakulima kuvamia eneo la wafugaji katika hifadhi hiyo ya Wembele na kuzuia Wafugaji kulisha mifugo yao, jambo lililokiuka makubaliano ya awali ya kila upande kubaki katika eneo lake.