Wafukuzwa kazi baada ya kutokea dosari kwenye tamasha

0
2046

Waziri wa Utamaduni wa Algeria, -Meriem Merdaci’s amejiuzulu wadhifa huo, zikiwa zimepita siku chache kufuatia watu Watano kufariki Dunia baada ya kukanyagana katika tamasha la muziki.

Tamasha hilo lilikua likitumbuizwa na Mwanamuziki nyota wa nchi hiyo Abderraouf Derradji maarufu kama Soolking, ambaye kwa sasa anaishi nje ya Algeria, lakini amekua akiimba nyimbo zinazoelezea maisha ambayo raia wa nchi hiyo wanayapitia kwa sasa.

Habari zaidi kutoka nchini Algeria zinasema kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini humo, – Abdelkader Kara Bouhadba naye amefukuzwa kazi kwa amri na Rais wa Mpito wa nchi hiyo Abdelkader Bensalah.

Hakuna sababu yoyote iliyotolewa ya kufukuzwa kazi kwa Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini Algeria, lakini baadhi ya maafisa wa serikali wamesema kuwa, ni kutokana na kasoro zilizojitokeza katika tamasha hilo.

Watu walioshuhudia tukio hilo la kukanyagana wamesema kuwa, lilianza baada ya maafisa usalama kuanza kuzuia umati wa watu uliotaka kuingia ndani ya uwanja, huku uwanja huo ukiwa umejaa.

Siku ya Ijumaa, Mkuu wa Taasisi inayohusika na Uandaaji wa Matamasha mbalimbali nchini Algeria,- Sami Benchik El Hocine naye alifukuzwa kazi kufuatia tukio hilo.

Raia wengi wa Algeria wanadai kuwa, maafisa wa vyombo vya usalama walizembea katika kutekeleza majukumu yao, hali iliyosababisha tukio hilo la kukanyagana, vifo vya watu hao Watano pamoja na majeruhi zaidi ya Ishirini.